Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire amewataka wanakandarasi wanaokarabati barabara ya Kebirigo-Mosobeti kumaliza ukarabati wa barabara hiyo kwa wakati ufaao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumapili, Bosire alisema kuwa yafaa wanakandarasi wanaokarabati barabara hiyo kumaliza shughuli hiyo kwa haraka ili kurahisisha usafiri.

“Ukarabati wa barabara ya Kebirigo-Mosobeti wastahili kumalizika kwa haraka ili kurahisisha usafiri hasa kwa wakulima wanaotumia barabara hiyo kusafirisha mazao yao," alisema Bosire.

Bosire aliongeza kwa kuisihi serikali ya Kaunti ya Nyamira kuchukua hatua zakufungua barabara zaidi kwenye eneo bunge la Kitutu Masaba ili kuwawezesha wakulima wa chai kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

"Baadhi ya maeneo katika eneo bunge langu hayapitiki kwasababu ya ukosefu wa barabara nzuri, hali inayofanya iwe vigumu kwa gari za kampuni za chai kufika katika mashamba ili kuchukua zao hilo. Hali hiyo husababisha chai kuharibika kabla ya kufika kwenye kampuni za usagaji chai," aliongezea Bosire.