Mbunge wa Kitutu Masaba iliyoko Kaunti ya Nyamira Timothy Bosire amewaomba Wawakilishi wa wadi zote katika kaunti hiyo kuzungumzia maendeleo ambayo serikali ya kaunti ya Nyamira imeyafanya.
Hii ni baada ya serikali ya kaunti hiyo kukiri kuwa tayari imefanya maendeleo mengi huku Mbunge Bosire akitumia mfano ambapo serikali ya kaunti hiyo ilisema kuwa iliweka mradi wa maji katika eneo la Nyangori, eneo bunge la Kitutu Masaba mradi ambao mbunge huyo amesema uliwekwa na East African community kupitia chama cha Lake Victoria Service Board na kukosoa serikali ya Nyamira kwa kuwadanganya wananchi.
Akizungumza mnamo siku ya Jumapili katika eneo bunge lake, Mbunge Bosire aliomba Wawakilishi wa wadi katika Kaunti ya Nyamira kuwajibikia kazi yao kikamilifu huku akisema kikatiba, Wawakilishi wa wadi wanastahili kuangalia yale serikali ya ugatuzi husika imetekeleza haswa kimaendeleo.
“Kuna ufisadi katika Kaunti ya Nyamira maana jinsi pesa za maendeleo zinatumika sio halali kamwe na wananchi sharti wapate kujua haki yao na mambo ya maendeleo maanake viongozi tulichaguliwa kufanya maendeleo kwa wananchi waliotupigia kura,” alisema Bosire, mbunge wa Kitutu Masaba.
Kwa upande wa wakazi hao walifurahishwa na matamshi ya Mbunge Bosire na kumuunga mkono kwa kusema serikali ya Nyamira haijafanya chochote kimaendeleo.
“Serikali ya Nyamira kwa kusema ukweli hatujafaidika nayo kabisa maana hamna maendeleo imefanyia,” alisema Peter Omwenga, mkazi wa Masaba.
Mbunge Bosire aliongeza kuwa ni jukumu la Wawakilishi wa wadi katika serikali ya Kaunti ya Nyamira kufanya kila juhudi kufuata yale yanatekelezwa na serikali hiyo kimaendeleo ili wananchi waweze kuridhika na uongozi.