Mbunge wa Homa-Bay Town Peter Kaluma ameziomba Serikali za ugatuzi pamoja na ile ya kitaifa kushirikiana pamoja na kufanya maendeleo katika sehemu zote nchini.
Akizungumza siku ya Jumanne katika ukumbi wa Gusii Cultural Hall mjini Kisii kwenye hafla ya kusanya maoni ya wanchi kuhusu pesa za hazina ustawi maeneo bunge (CDF), Mbunge Kaluma alisema sharti Serikali za ugatuzi na ile ya Kitaifa zishirikiane ili kufanya maendeleo zaidi katika sehemu zote za nchi.
“Serikali ya kitaifa na zile za kaunti zikiwa na ushirikiano sehemu zote za nchi zitanawiri zaidi kimaendeleo, kwa hiyo naomba tutangamane haswa katika sekta ya maendeleo,” alisema Mbunge Kaluma.
Aidha, Mbunge huyo alishukuru Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa maendeleo imefanya haswa katika sekta ya afya ikilinganishwa na serikali zingine za ugatuzi nchini.
“Serikali ya Gavana James Ongwae imejaribu sana haswa kwa sekta ya afya. Hiyo ndio maendeleo tunahitaji katika Kaunti zote,” aliongeza Kaluma.
Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na Mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi ambaye alisema kuwa Serikali zote zikishirikiana pamoja maendeleo yatafanyika zaidi katika sehemu za mashinani huku akiomba viongonzi wote kuweka siasa kando na kutilia maanani maendeleo.
“Hamna haja ya kuwa na siasa katika maendeleo. Heri tushirikiane ili wananchi wafurahie maendeleo ambayo tutayafanya sisi kama viongonzi wao,” alisema Moindi Mbunge wa Nyaribari Masaba.