Jengo la Mahakama ya Mombasa. Picha: Haramo Ali/ hivisasa.com

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa anatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya ulaghai juma lijaalo, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la kupinga kusomewa mashtaka hayo.

Ndegwa anadaiwa kutumia sahihi ya mtu aliyekufa kunyakua shamba la hekari zaidi ya nne katika eneo la Hindi, Kaunti ya Lamu mwaka 2013.

Mbunge huyo alikosa kusomewa mashtaka hayo ya ulaghai siku ya Jumatano baada ya wakili wake Jared Magolo kuomba mahakama muda wa siku tatu zaidi.Ndegwa aliwasilisha ombi mahakamani siku ya Ijumaa akipinga kufunguliwa mashtaka hayo katika Mahakama ya Mombasa.Kupitia kwa wakili wake Magolo, Ndegwa alisema kuwa mashtaka ya ulaghai yanayomkabili yanadaiwa kufanyika katika Kaunti ya Lamu, kwa hivyo ni kinyume cha sheria kushtakiwa Mombasa. Hata hivyo, Jaji Dora Chepkwony wa Mahakama kuu ya Mombasa, alitupilia mbali ombi hilo na kuagiza mbunge huyo kusomewa mashtaka katika Mahakama ya Mombasa siku ya Jumatatu.Ndegwa anakabiliwa pia na shtaka la kutengeza stakabadhi bandia ili kumwezesha kuuza shamba hilo kwa shilingi milioni nne.Aidha, anadaiwa kuwalipa wanunuzi wa shamba kupitia cheki bandia ya shilingi laki tano.Hapo awali, mbunge huyo pamoja na wafanyakazi sita wa hazina ya CDF ya Lamu Magharibi walishtakiwa kwa madai ya utumizi mbaya wa afisi na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja kila mmoja.