Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amesema kuwa atashirikiana na wabunge wenzake kuwasilisha mswada bungeni wa kushinikiza serikali za kaunti kununua vifaa vitakavyowasaidia waathiriwa wa saratani.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika kituo cha Coast Hospice, Nassir alisema kuwa licha ya masuala ya afya kugatuliwa kwa serikali za kaunti, bunge la taifa litasimama kidete kuhakikisha waathiriwa wa saratani wanapata usaidizi wanaohitaji.
“Nitawasilisha mswada bungeni kushinikiza serikali za kaunti kuweka vifaa vya kutibu maradhi haya ya saratani,” alisema Nassir.
Nassir aliwakabidhi waathiriwa hao dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo zenye kima cha shilingi laki mbili unusu, kabla ya kutembelea nyumba ya mayatima ya Mji wa Salama na kisha nyumba ya wazee ya Tudor.
Kwa upande wao, waathiriwa hao wakiongozwa na Khadija Ramadhan aliyeathirika na saratani ya titi, waliwahimiza wenzao wanaougua saratani kutumia dawa kama walivyoagizwa na daktari.
“Wale waathiriwa wenzangu ningependa kuwaomba tuendelee kutumia dawa kama tulivyoshauriwa na madaktari, na kwa wale ambao bado hawajapimwa basi tuweze kufika katika vituo vya afya kwa vipimo vya mara kwa mara,” alisema Bi Khadija.