Mbunge wa Njoro amedai maafisa wafisadi katika serikali ya Kaunti ya Nakuru wanashirikiana na wanosafirisha mazao kutoka shambani, kunyima serikali ya kaunti mamlioni ya pesa kutokana na kutolipa ushuru.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne mjini Nakuru, Joseph Kiuna alisema kwamba katika eneo bunge lake la Njoro, malori yanayobeba magunia ya viazi na karoti yanayopakiwa kupitia kiasi kwa muujibu wa sheria ya upakiaji hupita vizuizi vya barabarani baada ya hongo kutolewa.
Mbunge huyo alisema kwamba mazoea hayo yamepelekea wakulima kuteseka mikononi mwa mawakala ambao hujinufaisha pakubwa kifedha huku wakulima waliojibidiisha kupanda mazao hayo wakisalia kuhangaika wasijue la kufanya, kwa kupata mapato duni.
“Kuna kiwango kilichokubaliwa cha upakiaji wa kila zao na kutokana na hilo, ni lazima serikali ya Kaunti ya Nakuru ijibidiishe kuhakikisha hilo linaafikiwa,” alisema Kiuna.
Kiuna alidai kwamba maafisa wa polisi wanafanya kazi pamoja na maafisa wafisadi wa serikali ya Kaunti ya Nakuru ili kunyima serikali ya Kaunti ya Nakuru ushuru inayostahili kupata.
Mbunge huyo alidai kuwa visa hivyo vimekidhiri katika vizuizi vya Mau, Narok na Mauche mjini Njoro.
Kwa sasa, mbunge huyo amemtaka Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kuwahusisha viongozi waliochaguliwa katika kuendeleza shughuli za kila siku za kaunti, kwa kuwa gavana hawezi kuendeleza shughuli hizo peke yake.
Kiuna alisema kuwa mawaidha kutoka kwa viongozi waliochaguliwa ni muhimu katika kuleta maendeleo kwenye kaunti.
Pamoja na hayo, amemtaka Gavana Mbugua kuwahusisha katika mikutano ya mara kwa mara ili waweze kujua maswala yanayowatatiza wakazi wa kaunti hii.