Mbunge wa Molo Jacob Macharia amepongeza serikali Kwa kumaliza mzozo wa ardhi katika eneo bunge lake.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza Jumatatu katika wadi ya Turi, Molo, Macharia alisema kuwa eneo la Molo katika miaka ya awali limekumbwa na mizozo ya ardhi lakini sasa kuna utulivu baada ya serikali kupeana hati miliki za ardhi.

"Tunajua Molo imekuwa ikipokea wageni wengi wanaotoroka machafuko huko Kuresoi na wanapokuja kunakuwa na mizozo ya ardhi lakini sasa tunaeza sema kuna utulivu na naipongeza tu serikali,"alisema Macharia.

Wakati huo huo, alitoa wito kwa serikali kuingilia kati swala la mashamba kama vile Managu na Migaa ili suluhu ipatikane kama ilivyotatuliwa ile ya Ndimu Molo.

Vilevile, aliitaka serikali ya kaunti ya Nakuru kuwasaidia wakaazi wa Kasarani ambao wana deni kubwa ya ada za ardhi.

"Langu ni ombi tu Kwa serikali ya kaunti kwamba wajaribu kuangalia namna watasaidia wakaazi wa Kasarani Molo ambao wana deni kubwa ya ada za ardhi,"alisema Macharia.