Mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi amewaomba wanafunzi kutumia njia mwafaka kutuma maombi ya kupata pesa za 'bursary' za kuwakimu katika kulipia karo na kukoma kumtumia ujumbe za kumwomba pesa hizo.
Akiongea leo (Jumanne) asubuhi alipomtembelea mkurugenzi mkuu wa elimu kwenye Kaunti ya Kisii, Moindi aliwataka wanafunzi wa shule za upili, Vyuo Vikuu na Taasisi kuwa na utaratibu nzuri wa kutuma maombi ya kupata hela za kulipia karo na kuongeza kuwa hahusiki kamwe kutoa pesa hiyo kwani kuna kamati iliyoteuliwa ya kushughulikia pesa hizo.
Mheshimiwa Moindi aliwaonya baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe mfupi kwenye simu yake ambapo alitoa mfano wa mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Kisii ambaye alimtumia ujumbe wa kumshurutisha amlipie pesa.
"Kuna njia nzuri za kutuma maombi ya kupata pesa za karo, nawashauri vijana mje katika ofisi ya CDF ili kuelekezwa jinsi ya kutuma maombi ya kupata fedha hizo," alishauri Mbunge Moindi.
Mbunge huyo pia alisema kuwa yupo tayari kusaidia jamii ya Mogusii kwa jumla kuafikia azimio la kuboresha elimu ya wanafunzi wote kutoka eneo lake la Bunge na Kaunti ya Kisii kwa jumla.
"Elimu ndio malengo yangu katika nafasi hii ya uongozi, naomba tushirikiane pamoja na wakaazi wote na viongozi wa Kisii kuinua elimu,” alihoji Mbunge huyo.