Mbunge wa Mugirango Kusini katika Kaunti ya Kisii Manson Nyamweya ametangaza kuwa ifikapo mwaka wa 2017 atakiwania kiti cha ugavana katika Kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akionga na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Ijumaa, Mbunge Manson alisema kuwa kuna baadhi ya maendeleo ambayo yanastahili kufanywa na Serikali ya Kaunti ambayo hayajafanywa na kusema akichukuwa wadhifa huo atazishughulikia kikamilifu kwa manufaa ya wakaazi wa Kisii.

Wakati uo huo, Mbunge huyo alisema kuwa baadhi ya zahanati katika eneo Bunge lake hazina dawa za kutosha ambazo zinastahilIi kufadhiliwa na Serikali ya kanti hiyo.

Miongoni mwa zahanati alizozitaja ni ile ya Nyamarambe, Moticho na Etago, jambo ambalo halimfurahishi hasa katika sekta ya afya jinsi inashughulikiwa na serikali ya Kaunti hiyo.

Aidha, Mbunge huyo amewahakikishia wakaazi wa Mugirango Kusini kuwa atafanya maendeleo katika eneo hilo mpaka mwaka wa 2017 na kukana kuwa si kampeini ameanzisha.

“Nitawafanyia maendeleo watu wangu mpaka uchaguzi ujao ufike, lakini nakimezea mate kiti hicho cha ugavana ili nifanyie watu wa Kaunti nzima ya Kisii maendeleo,” alidokeza Nyamweya.

Mbunge huyo aliwaomba viongozi wote wa eneo la Kisii kushirikiana na kuungana pamoja kama jamii ya Wakisii na kuwafayia maendeleo wakaazi wa maeneo hayo.

“Nawaomba viongonzi tuweke tofauti zetu za kisiasa kando, tufanye maendeleo kwa wananchi wote kwa njia ya haki na usawa,” aliongezea Nyamweya.

Kwa upande mwingine wakaazi wa eneo hilo wamemwomba Mbunge huyo kuzitengeneza barabara alizowaahidi kuwa angezitengeneza hapo mbeleni.

“Tunamuomba Mbunge wetu Nyamweya kabla hajakiwania kiti cha ugavana ambacho anakisema atufanyie maendeleo haswa kuweka lami barabara za eneo hili. Tunamtaka amalize kazi yake tuliyomchagulia kufanya kama Mbunge, kisha baadaye atakiwania kiti anachohitaji kwani uamuzi ni wake,” alihoji Amos Kerama mkaazi wa Tabaka ipatikanayo katika eneo Bunge la Mugirango Kusini.