Waandishi wa Habari katika maeneo ya Gusii wametiwa motisha baada ya Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong'i kuwaahidi kuwa atahakikisha wamelindwa dhidi ya kudhulumiwa na Maafisa wa Polisi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea siku ya Alhamisi usiku nje ya Kituo cha Polisi cha Central mjini Kisii, Mbunge Tong’i aliwahakikishia waandishi wa Habari hao ambao walikusanyika nje ya kituo hicho baada ya ripota wa Nation na mwenzake kutoka Standard kuvamiwa na Polisi Alhamisi walipokuwa wakipiga picha kwenye fujo ya wanafunzi wa Gusii waliokuwa wakiandamana kufuatia ajali ya barabara iliyosababisha vifo vya wenzao.

"Hilo suala la kunyanyaswa nitalishughulikia mimi binafsi na sharti hawa Polisi waheshimu sheria na kufanya kazi yao bila kudhulumu yeyote,” alisema Mbunge Tong’i.

Waandishi wa Habari kutoka Kaunti ya Kisii wamekuwa wakilalamikia dhuluma dhidi yao kutoka kwa baadhi ya Maafisa wa Polisi ambao wanadai kuwa Waandishi hao wanaandika mambo mabaya kuwahusu.

Hii inajiri baada ya Polisi mmoja kutoka Kituo hicho cha Central mjini Kisii kudaiwa kumtishia Mwandishi wa Habari wa gazeti la The Star kwa madai kuwa 'aliwapaka matope' suala ambalo limesababisha uhusiano mbaya baina yao na Maafisa wa Polisi.