Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amewahimiza maafisa wa kusajili wapigaji kura kutembelea shule na vituo vya kibiashara ili kuwasajili vijana waliotimiza miaka 18.
Akihutubu katika uwanja wa michezo wa Bahati kwenye sherehe za madaraka siku ya Jumatatu, mbunge huyo alisema kuna vijana wengi katika eneo hilo ambao hawajasajiliwa kama wapiga kura kwa sababu hawana vitambulisho licha ya kufikisha umri unao hitajika.
“Usajili wa wapiga kura tayari umeanza na maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC wamekuwa wakitembelea vituo vya kibiashara wakisajili wapiga kura. Hata hivyo nimepata ripoti kuwa ni watu wachache mno wanao jitokeza kusajiliwa. Sababu kuu ni kuwa hawana vitambulisho ambvyo ni lazima ili uweze kusajiliwa,” Ngunjiri alisema.
Mbunge huyo aidha, aliwahimiza wakaazi wa Bahati kushirikiana na machifu pamoja na maafisa wengi wa utawala ili kuangamiza upishi na unywaji wa vileo haramu ambao umekuwa kikwazo kikuu cha maendeleo miongoni mwa vijana.
Wakati huo huo, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini Geofrey Kithinji Ithai akihutubu kwenye sherehe hizo aliwataka machifu kuwa waangalifu na makini kwa wakazi wanao pata makazi katika maeneo yao wasije wakawa ni magaidi.
“Vijana12 kutoka kila kata wamechaguliwa kupewa mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja kuhusu usalama wa jamii. Hatua hii inanuiwa kuchagia pakubwa katika kuimarisha usalama katika eneo Bunge hili. Baada ya kukamilisha masomo hayo, vijana hao wanatarajiwa kuwafunza wengine kule vijijini,” afisa huyo wa utawala aliongeza.