Mbunge wa Bobasi Stephen Manoti amekanusha madai kwamba pesa za ustawi wa maeneo bunge maarufu kama CDF za mwaka 2013/2014, za eneo bunge lake zitarejeshwa katika hazina ya kitaifa kwa kutotumika.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa, Manoti alikana madai hayo na kusema kuwa fedha hizo zilichelewa kutolewa na serikali kuu kufuatia kesi iliyokuwa mahakamani.

“Kuna uvumi wa uongo unaoenezwa kuwa pesa za CDF za eneo bunge letu za mwaka 2013/2014 zitarejeshwa katika serikali kuu baada ya kutotumika. Pesa hizo zilitolewa kama zimechelewa kwa sababu kulikuwa na kesi mahakamani iliyowekwa na mwakilishi mmoja wa kaunti,” alisema Manoti.

Alithibitisha kuwa hazina ya eneo bunge hilo imepatiwa kiasi cha Sh32 milioni na wanatarajia fedha zaidi. 

Wakaazi wa eneo bunge hilo wamekuwa wakinung’unika kuhusu matumizi ya pesa za ustawi wa maeneo bunge, ambapo wanadai mbunge wao amezembea inayopelekea pesa hizo kurejeshwa katika serikali kuu.

Kulingana na wakaazi walioongea na mwandishi huyu, mbunge huyo hajafanya maendeleo yoyote na fedha za CDF tangu achaguliwe, na hivyo wamemtaka azinduke na kutekeleza majukumu yake.

“Tunampenda mbunge wetu lakini amezembea sana na hajafanya lolote tangu tumchague. Inakuwaje fedha za CDF zirejeshwe kwa serikali kuu ilhali tuna mahitaji mengi,” alisema James Ondabu, mkaazi wa wadi ya Bointang’are.