Mbunge wa Borabu Ben Momanyi amesema kuwa iwapo serikali ya Jubilee itashughulikia maslahi ya wakazi wa kaunti ya Nyamira, basi wabunge wa eneo hilo wataiunga mkono serikali kwenye uchaguzi ujao.
Akiwahutubia wakazi wa Kebirigo siku ya Jumatano wakati waliopoandamana na rais Uhuru Kenyatta kwenye ziara yake eneo hilo, Momanyi alisema kuwa wakazi wa Nyamira wataiunga mkono serikali ya Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao iwapo miradi ya maendeleo itatekelezwa eneo hilo.
"Mheshimiwa Rais hawa watu wa Nyamira wanakupenda sana na ndio maana wamejitokeza kwa wingi ili kukukaribisha, na ukweli ni kwamba iwapo utatuangalia vizuri, watu wa Nyamira hawataenda kombo tena," alisema Momanyi.
Momanyi aidha alimshukuru rais Kenyatta kwa kujitolea kwa serikali yake ili kuzindua ujenzi wa barabara kuu ya Kebirigo-Mosobeti, hali aliyosema kwamba itawasaidia wakazi wa eneo hilo kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
"Barabara ambazo tumekuwa tukitaka zitengezwe ndizo hizi anazozindua rais Kenyatta na kwa kweli pindi zitakapokamilika wakazi wa maeneo haya hasa wakulima watakuwa na urahisi wa kusafirisha mazao yao," aliongezea Momanyi.