Mbunge wa eneo bunge la Borabu Ben Momanyi amejitokeza kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwaomba wakenya msamaha kutokana na matamshi yake kuhusu mahakama ya ICC.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa kule Mokomoni siku ya Jumapili, Momanyi aliyataja matamshi ya Rais Kenyatta kwamba hamna mkenya yeyote atakayewasilishwa kwenye mahakama hiyo kama mzaha.
"Ni jambo la kushangaza kwamba rais Uhuru Kenyatta anaweza idhalilisha mahakama ya kesi za jinai kwa kusema kuwa hamna mkenya yeyote atakayewasilishwa kwenye mahakama hiyo ili kujibu mashtaka kuhusiana na kesi za jinai na sharti awaombe wakenya msamaha," alisema Momanyi.
Momanyi aidha alishangazwa ni kwa sababu gani rais Kenyatta haiamini mahakama ya ICC ikizingatiwa kwamba mahakama hiyo ndiyo iliyowaondolea mashtaka naibu rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang.
"Inakuaje kwamba rais na naibu wake waliandaa hafla ya kusherehekea maamuzi ya mahakama ya ICC kuhusiana na kutupiliwa mbali kesi za Ruto na Sang, halafu iwe kwamba Rais Kenyatta anachochea wakenya dhidi ya mahakama hiyo," aliuliza Momanyi.
Haya yanajiri baada ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto kutaja wazi kule Nakuru siku ya Jumamosi kwamba hamna mkenya yeyote atakayewasilishwa kwenye mahakama ya kushughulikia kesi za jinai kule Hague, Uholanzi.