Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi katika hafla ya awali. [Picha/ kbctv.co.ke]
Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amefikishwa mbele ya mahakama kwa madai ya kuzua fujo na kutatiza uchaguzi wa mchujo wa chama cha ODM.Mwinyi anadaiwa kuvunja madebe ya kupigia kura katika baadhi ya vituo wakati wa zoezi hilo siku ya Jumamosi.Hata hivyo, Mwinyi hakusomewa mashtaka baada ya Hakimu Erick Makori kutaka kupewa muda ili kubaini iwapo madai yanayomkabili mbunge huyo yanaambatana na sheria za uchaguzi.Mahakama itatoa uamuzi tarehe Mei 8.Haya yanajiri huku mpinzani wake Goshi Juma Ali akikitaka chama cha ODM kumpiga marufuku Mwinyi kwa kutatiza uchaguzi huo wa mchujo.Akizungumza na wanahabari katika shule ya msingi ya Bomu, Goshi alisema kuwa kulingana na sheria za chama hicho, mwanachama anapozua rabsha wakati wa uchaguzi yuafaa kupigwa marufuku.Mwinyi alitiwa mbaroni na maafisa wa polisi baada ya kisa hicho na hatimaye kuachiliwa huru kwa dhamana.Wawili hao walikuwa wakipigania tiketi ya chama cha ODM kuwania kiti cha eneo bunge la Changamwe kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti nane.