Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba, kaunti ya Nyamira Timothy Bosire ametishia kuongoza maandamano kulalamikia ‘uongonzi mbaya’ wa kaunti ya Nyamira.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea mnamo siku ya Alhamisi katika uwanja wa shule ya msingi ya Rikenye iliyoko wadi ya Rigoma, kaunti ya Nyamira wakati alikuwa anakabidhi shule hiyo pesa ya ustawi maeneo bunge CDF, Bosire alisema kuwa usimamizi wa kaunti hiyo haujatenda yale waliahidi.

“Wananchi wengi kutoka eneo bunge hili wanauliza kaunti ziko na maana gani, maana hawajafaidika na chochote kutoka kaunti hii ya Nyamira. Wananchi wako na shida nyingi na uongozi haujasaidia katika jambo lolote,” alisema Bosire.

“Hakuna hospitali na shule ambazo zimetengenezwa, na uongozi wa kaunti una billioni 4.5, pesa ambazo zingetumiwa kuleta maendeleo, lazima tuwakalishe chini watueleze yale wametekeleza na kimaendeleo kama serikali ya Nyamira,” aliongeza Bosire.

Aidha, mbunge huyo alisema tangu serikali za kaunti zianzishwe miaka mitatu iliyopita, serikali ya Nyamira ndio imerudi nyuma kimaendeleo, huku akitoa mfano wa kaunti ya Kisii ambayo ‘imeendelea’ sana.

“Mbona kaunti ya Nyamira isifanye maendeleo kama kaunti zingine ambazo zimetumia fedha vizuri na kufanya maendeleo?” aliuliza Bosire.