Mbunge wa eneo bunge la Mugirango kaskazini Charles Geni amewapa wakuu wa usalama katika kaunti ya Nyamira makataa ya wiki moja kuwakamata na kuwashtaki washukiwa wa mauaji ya mme na mkewe katika kijiji cha Gekonge.
Hali ya majonzi na simanzi ilitanda katika kijiji hicho wakati maelfu ya waombolezaji walimiminika kuomboleza vifo vya wawili hao ambapo kila aliyepata fursa kuzungumza alitaja kuwa washukiwa hao wanajulikana katika maeneo hayo na kuwa polisi wameshindwa kuwashtaki kila wanapowakamata.
Geni amesema kuwa mbali na washukiwa hao ambao wamekuwa wakiwaua wenyeji kinyama kukamatwa, wamekuwa wakiachiliwa punde tu ya kukamatwa na kudai wanalipiwa pesa na wanasiasa fulani na kurejea kuendelea kuwaangaisha wenyeji.
"Nawapa wakuu wa usalama katika kaunti hii wiki moja kuwashika na kuwashtaki wahusika wa mauaji haya la sivyo waende penye wanataka kuhudumia wananchi," alisema Geni.
Aidha wanasiasa walipata fursa ya kipekee kujiuza kwenye mazishi hayo ya mzee Geofrey Kemonde na mkewe ambayo yalitatizwa na mvua kubwa ambayo ilinyesha katika sehemu hiyo japo haikuwanyima wanasiasa hao nafasi ya kuhutubia umati huo mkubwa wa waombolezaji.
Wagombezi kadhaa wa kiti cha ugavana wa kaunti hiyo akiwemo Charles Mochama, Mwancha Okioma miongoni mwa wengine walitafuta uungwaji wa mkono huku wakilaani kitendo hicho cha mauaji hayo ya kikatili.
Kifo cha wawili hao kinafikisha idadi ya waliouawa kufikia sita kwa muda wa miezi mitatu iliyopita wakiwemo maafisa wawili wa nyumba kumi.