Mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir amekashifu mbinu zinazotumika na maafisa wa polisi katika vita dhidi ya ugaidi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Nassir alisema kuwa mbinu hizo zimechangia uhasama mkubwa katika jamii bila ya polisi kutimiza lengo lao.

Nassir alidokeza kuwa licha ya kuwatia mbaroni watu wanaoshukiwa kuwa magaidi na kisha baadaye kuwapata bila ya hatia, polisi hawajawajibika kuomba msamaha kwa waathiriwa kwa kuwachafulia majina.

Alisisitiza kuwa vijana wengi wanatiwa mbaroni kiholela pasi kuwa na hatia yoyote.

Mbunge huyo aliyasema haya kwenye kikao cha pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu jijini Mombasa.

Haya yanajiri huku takwimu kutoka tume ya kitaifa ya utetezi wa haki za binadamu zikionyesha kuwa jumla ya visa 125 vya watu kupotea kwa njia ya kutananisha viliripotiwa katika mwaka 2014/2015 ambapo 81 kati yao hawajulikani walipo kufikia sasa.