Kwa mara ya kwanza mbunge wa eneo bunge la Nyaribari chache Richard Tong'i amejitokeza kuzungumzia suala la mzozo wa kimpaka kule Keroka kati ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye uwanja wa shule ya upili ya Nyabikomu siku ya Ijumaa, Tong'i alizishtumu serikali za kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kwa kuzembea kusuluhisha mzozo huo wa kimpaka, hali aliyosema inaendelea kuchochea ghasia katika eneo hilo. 

"Ni aibu kwamba watu wa jamii moja wanazozonia mji wa Keroka huku kila mtu akisema kuwa eneo hilo lipo kwenye himaya yao na kwa kweli hali hii inatatokana na gavana Nyagarama na Ongwae kutufeli pakubwa," alisema Tong'i. 

Mbunge huyo aidha aliwataka magavana hao wawili kuketi na kufanya mazungumzo ya kumaliza mzozo huo wa kimpaka kwa haraka. 

"Ni jukumu la magavana hawa wawili kuwaunganisha watu wa kaunti zao na ndio maana wakubali kuzika tofauti zao ili kuketii pamoja na kusuluhisha mzozo huo wa kimpaka kwa haraka iwapo wanataka amani iwepo," alihoji Tong'i.