Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari chache Richard Tong’i amewapa changamoto viongozi kutoka kaunti ya Kisii kujitolea kwa kuwapa wanafunzi msaada wa kielimu wanapohitaji.
Tong’I alikuwa akiongea siku ya Jumatatu katika hafla ya kutembelea miradi ya shule za eneo bunge lake, katika sehemu ya Kiogoro, ambapo alitoa ufadhili wa kifedha na vitabu kwa shule mbali mbali za eneo hilo ambapo aliwaomba viongozi wengine kufuata mfano huo na kuwasaidia wanafunzi kwa masomo na talanta.
Hafla hiyo iliwakutanisha viongozi mbali mbali kutoka eneo hilo ambao waliwania viti vya wadi na vile vya ubunge pamoja na wazazi, na walikubaliana kwa pamoja kuunga mkono miradi ya elimu ili kuimarisha viwango vya sehemu hiyo ambavyo vimedorora.
“Nipo tayari kuwasaidia wanafunzi werevu kuendelea na elimu hadi vyuo vikuu na wale ambao wanajitahidi katika masuala ya talanta mbali mbali tutawapa msaada ili wajiendeleze katika maisha ya baadaye,” alihoji.
Kwingineko, kiongozi mmoja ambaye pia ni mfanyabiashara katika mji wa Kisii Bwa Wilfred Bosire aliahidi kujitolea kutoa shilingi elfu mia moja kwa kila shule ambayo itaboresha matokeo yake ya kitaifa kwa alama wastani, na kutoa shilingi elfu ishirini kwa kila mwanafunzi ambaye atafanya vizuri kwa mitihani hiyo.
“Fanya bidii mpate matokeo mazuri zaidi na nitatoa elfu 100 kwa kila shule ambayo itafanya vizuri na shilingi elfu 20 kwa kila mwanafunzi ambaye ataibuka kidedea,” alihoji bwana Bosire.