Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong'i alikamilisha maadhimisho ya siku kuu ya Madaraka katika sinema kwa kuungana na vijana wa mtaa kula kwenye kibanda kimoja kilichoko nje ya Uga wa michiezo wa Gusii Green kulikoandaliwa hafla hizo.
Mbunge huyo alisema kuwa alichukua hatua hiyo kula na vijana wa mtaa ili kuwaonyesha umoja na ushirikiano na wasione kuwa wao kama Wabunge hula tu katika mikahawa mikubwa tu, bali wanakumbuka mikahawa midogo akisema kuwa hapo ndio walianzia.
Mwenye mkahawa huo Jastus Omare hakuficha furaha yake kuhusu uamuzi huo wa ‘ungwana' alionyesha Mbunge huyo kwa kula katika Hoteli yake huku akisema kuwa kitendo hicho kimemuuinua kimapato kwani vijana ambao walikuwa wamemfuata mheshimiwa huyo walinunuliwa vyakula mbali mbali kwenye mkahawa huo.
"Namshukuru Mbunge Tong'i kwa kuchagua hoteli yangu. Biashara imekuwa nzuri leo na nawaomba viongozi wengine kufuata mkondo huo kwa kula na watu wa ngazi ya chini," alisema mwenye hoteli hiyo.
Mbunge huyo aliwaahidi vijana wa kuzoa taka kwenye maeneo yanayozingira uga huo ambao hujiita Chache Clean our Town Youth Group kuwa atahakikisha masilahi yao yanashughulikiwa haswa kwa kupewa vifaa vya kufanyia kazi ya usafi.