Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta mteule wa Mombasa Emma Mbura amekosoa hatua ya Gideon Mung’aro kuondolewa katika wadhfa wake kama mwenyekiti wa muungano wa wabunge wa pwani.

Seneta Mbura alipinga akisema viongozi wa pwani wanafaa kushirikiana pamoja kuleta maendeleo na kuongeza kuwa hatua hiyo huenda ikaleta mgawanyiko miongoni mwao.

Aikongea mjini Nairobi siku ya Ijumaa, Mbura alisema kuwa eneo la pwani limeachwa nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu kwa kukosa kushirikiana na serikali.

“Kwa miaka mingi tumekataa kuunga mkono serikali na tumeumia vya kutosha, ilikuwa ni sawa tufanye kazi na serikali ndio tuweze kuleta maendeleo kwetu pwani.” Alisema seneta Mbura.

Wakati huo huo Mbura alisema kuwa mambo ya siasa yaliisha wakati wa uchaguzi na kilichosalia ni kufanya kazi bila kuangalia chama.

“Hata kama kuna ODM, tulipiga kura 2013 na siasa zikaisha hapo kilichobaki ni kufanya kazi kwa pamoja.” Aliongeza Mbura.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mapema wiki hii siasa zilionekana kuchukua nafasi yake kwani viongozi wote waliochaguliwa katika muungano huo wanatokea katika mrengo mmoja wa CORD.

Wabunge waliohasi mrengo huo walitupwa kando katika uchaguzi huo akiwemo Gideon Mung’aro na mwenzake wa Lungalunga Khatib Mwashetani.

Wadhfa wa mwenyekiti ulichukuliwa na mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga.