Hatua ya baadhi ya wabunge kutaka kuwasilisha mswaada wa kuwazuia maseneta kugombea ugavana nchini imepingwa vikali.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Seneta Mteule wa Kaunti ya Mombasa Emma Mbura amesema kuwa iwapo mswada huo utapelekwa bungeni na kupitishwa, basi utakuwa unakiuka haki za kikatiba nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mbura alisema kuwa kila mtu ana uhuru wa kugombea kiti chochote anachotaka mradi tu awe na stakabadhi hitajika.

Mbura aliwapuuzilia mbali wabunge waliotoa pendekezo hilo, kwa kusema kuwa wabunge hao wana malengo binafsi.

"Hatuwezi kukubali kuona bunge la kitaifa likihujumu ugatuzi na katiba ya nchi. Ikiwa wao wanataka kuwania ugavana, wanaruhusiwa na wala sio kupitisha mswada usio kuwa na umuhimu wowote kwa wananchi,” alisema Mbura.

Kauli ya Seneta Mbura inajiri huku baadhi ya maseneta kutoka kaunti mbalimbali wakionyesha ari ya kugombea kiti hicho cha ugavana kwenye uchaguzi mkuu ujao.