Mwakilishi wa wadi ya Kisii ya kati kaunti ya Wilfred Monyenye amekashifu kitendo cha watoza ushuru katika soko la Keroka kutiwa mbaroni hiyo jana kwa kile kilichosemekana kuwa mzozo wa mpaka kati ya kaunti hiyo na ile ya Nyamira.
Hii ni baada ya watoza ushuru sita kutiwa mbaroni huku wanne wakiwa wa kaunti ya Kisii na wawili wa kaunti ya Nyamira, Watoza ushuru hao walitiwa mbaroni kwa kukusanya ushuru mahala tofauti kando na pale wamekubaliwa.
Akizungumza mjini Kisii Monyenye alikashifu kitendo hicho na kusema hakuna haja kwa mzozo huo kuendelea huku akiomba watoza ushuru wa kaunti ya Nyamira na wale wa Kisii kutoza ushuru penye wanastahili na kutovuka mpaka uliowekwa.
“Ni haki kwa watoza ushuru wa Kisii kutoza ushuru mahali walipewa laikini ikiwa wale wa Nyamira wanavukia mipaka hadi kaunti ya Kisii ni kinyume na sheria sharti mpaka ufuatwe bila ubaguzi,” alisema Monyenye.
Aidha, Monyenye alimkosoa mkuu wa polisi katika kituo cha Ramasha kwa kuonyesha ubaguzi kwa kupendelea sana watoza ushuru wa kaunti ya Nyamira.
Watoza ushuru hao walifikishwa katika kituo cha polisi cha Kisii kisha wakaachiliwa kwa bondi ya shillingi 10,000 kila mmoja huku wakisubiri kufikishwa mahakamani.