Share news tips with us here at Hivisasa

Hoja iliyowasilishwa katika bunge la kaunti la kuwaondoa makahaba mjini Mombasa inaendela kuibua hisia tofauti miongoni mwa viongozi na wananchi kwa ujumla.

Baadhi ya viongozi katika bunge hilo wameonekana kuunga mkono pendekezo hilo huku baadhi yao wakipinga hoja hiyo kwa madai kwamba inakiuka haki za binadamu.

Mwakilishi wadi mteule Mary Akinyi alipinga hoja hiyo ya kutaka kuwaondoa makahaba hao, kwa kusema kuwa kuna njia nyingi za kuwasaidia bila kuwafurusha kabisa.

Akizungumza na wanahabari baada ya vikao vya bunge siku ya Jumanne, Akinyi aliishauri Idara ya vijana, jinsia na michezo kuchukua jukumu la kuwasaidia wasichana hao.

“Inafaa waanze kuwaelimisha ili waache biashara hiyo kwa kuwafungulia biashara mbadala. Ikiwa ni mambo tu ya kuwafurusha, basi hatua hiyo italeta shida kwa sababu watakuwa wananyimwa haki zao,” alisema Akinyi.

Aidha, Akinyi alisema kwamba ni vigumu kukomesha biashara hiyo ya ukahaba kabisa kwani wapo wasichana wengi wanayoitegemea.

“Watu wengi wamenufaika kutokana na biashara ya ukahaba. Weingi wamejiendeleza na wengine hata wamesoma kupitia kazi hiyo,” alisema Akinyi.

Hoja hiyo iliyopendekeza makahaba kuondolewa mjini Mombasa iliwasilishwa bungeni na Mwakilishi wa Wadi ya Tononoka Saad Faraj, kwa madai kwamba wanaharibia sifa mji huo wa kitalii.