Wenyeji wanaochimba mawe kwenye mashamba yao na kuharibu barabara katika wadi ya Bahati, watachukuliwa hatua kali za kisheria kulingana na Peter Nderitu, MCA wa wadi hiyo.
Hii ni baada ya wakaazi wa eneo haswa Jacaranda kulalamikia uharibifu wa barabara unaotekelezwa na watu wanaokodi karakakana katika mashamba ya watu, unaofanya barabara hizo kukatika.
Wakiongea na mwandishi huyu Jumanne katika eneo la Wanyororo B, wakiongozwa na Samwel Kamau Chege, walisema sasa wanahofia usalama wa watoto wao, mifugo na mafuriko, kutokana na hatari inayoletwa na mashimo yanayoachwa wazi na wachimbaji hao wa mawe.
"Sasa hata magari yanayokujia mawe hayo hayako salama kwa sababu watu wanaochimba mawe wamechimba hata nusu ya barabara. Hayo ndiyo mashimo yanatumiwa na wahalifu kujificha na wanaweza kutushambulia," Chege alisema..
Naye Roseline Gathega alisema watu wanaoharibu barabara hizo wanafanya iwe vigumu kwa maendeleo kufanywa na serikali ya kaunti.
“Kuna wakati barabara zikiharibika, tulikuwa tunapeleka akina mama kujifungua hospitalini lakini wanajifungulia njiani. Sasa wanaochimba mawe wameharibu hata zaidi” Gathega aliongeza.
Beatrice Wambui hata hivyo alipongeza serikali ya kaunti ya Nakuru chini ya gavana Kinuthia Mbugua, na MCA Nderitu kwa kujikakamua kupeleka maendeleo mashinani.
“Sitavumilia watu wanaovunja sheria. Kama una karakana unachimba kwako, hakikisha unabakisha sehemu ya mita 2 hadi 5 mbali na barabara kama sheria isemavyo. La sivyo utakamatwa", akasema MCA Nderitu
Chifu wa eneo hilo Wakahiu Macharia, alisema wachimbaji kadhaa wa mawe wamekamatwa kwa kuharibu barabara.