Bunge la Kaunti ya Mombasa limelaumiwa kwa kile kinachotajwa kama ni kushindwa kuboresha hali ya maisha katika jamii.
Akiongea katika eneo la Changamwe mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mwanaharakati wa masuala ya maendeleo katika eneo bunge hilo Onesmus Nganga, alisema kuwa wawakilishi wa bunge hilo wanapaswa kuyashughulikia matatizo yanayowakumba wakaazi wa mashinani.
Nganga anasema kinyume na hali ilivyo katika maeneo mengine nchini ambako viongozi wao wamewajibika, Kaunti ya Mombasa imesalia nyuma kimaendeleo.
Mwanaharakati huyo wa masuala ya maendeleo katika eneo la Changamwe, hata hivyo aliwataka wakaazi wa eneo hilo wahakikishe kwamba wanatekeleza mageuzi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
“Bunge la kaunti ya Mombasa hasa wawakilishi wameshindwa kuwajibikia majukumu yao katika maswala ya maendeleo na kufuja tu fedha za umma ndio maana tunawaambia wakaazi wafanye mageuzi wakati wa uchaguzi mkuu ujao," alisema Ngang'a.