Mchakato wa uchambuzi wa bajeti ya Kaunti ya Nakuru umeanza huku wakaazi wakitakiwa kujitokeza na kutoa mchango wao.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika ukumbi wa kijamii wa Kivumbini katika eneo la Nakuru Mashariki, Francis Shinali, kutoka muungano wa 'Nakuru Neighbourhood Association' alisema kuwa in wajibu wa mwananchi kuhusika katika maswala ya bajeti kwa mujibu wa katiba.
"Katiba iko wazi kuhusu wananchi kuhusishwa katika uongozi na maswala ya miradi inayotengewa fedha katika bajeti, kwa kupewa fursa ya kutoa maoni yao,” alisema Shinali.
Aidha, Shinali alisema kuwa kwa ushirikiano na mashirika mengine, watazidi kuelimisha jamii kuhusu vipengee vinavyohusu mwananchi kwenye katiba.
Alitoa wito kwa vijana na akina mama kujitokeza kila mara mikutano ya uhamasisho inapoandaliwa.