Ukitazama kwa umbali utadhania kwamba ni vuta ni kuvute ya vita. La, ni mchezo uliokua maarufu sana katika siku za kale ambao ulitumiwa na mababu kujiimarisha kiafia na hata kujipima nguvu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Ni mchezo wa kuvuta kamba ambao bado ungali unaendelezwa miongoni mwa jamii za Luo na nyinginezo chache nchini ambazo bado zingali zinadumisha maadili kwa kuendeleza mila na desturi za jamii hizo.

Hapa ni wanaume na wanawake wakipimana nguvu kwenye mchezo wa kuvuta kamba ambao uliandaliwa mnamo siku ya Jumatano katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Pap-Onditi, Tarafa ya Nyakach kwenye hafla moja ya kuchangisha pesa za hazina ya maendeleo ya kikundi kimoja cha wazee wa hapa.

Kwenye hafla hiyo wakaazi wa eneo hilo waliombwa kutunza mila zao ili kuhusisha na kuendeleza utu bora miongoni mwa jamii za kutoka eneo hilo ili kukuza vyema kizazi kipya ambacho kimepotoka kwa kuiga tamaduni za kigeni ambazo haziambatani na maadili ya kiafrika.

Akihutubu kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa wazee wa Ukoo wa Nyakach Dalmas Okech alisema kuwa kizazi kipya kitaangamia iwapo mila na tamaduni za kikwetu zitapuuzwa.

“Jamani hatuna jamii siku zijazo iwapo maadili yetu yatasambaratika. Tumekiacha kizazi hiki kukumbatia tamaduni za kigeni, ilhali tunazo mila zetu ambazo hutunza jamii kwa maadili mema,” alisema Okech.

Aidha kiongozi huyo wa jamii alihoji kua vijana wanavalia nusu uchi na kujifunza matamshi yasiyoeleweka yaliyo na maneno yenye kiburi, hali ambayo inaharibu kabisa kisasi cha leo.