Utafiti unaonyesha kwamba takriban watu 1000 hufariki kila siku nchini Kenya kutokana na virusi vya ukimwi.
Hali hii ya kuhuzunisha hupelekea mamia ya watoto kuachwa mayatima baada ya wazazi wao kufariki, huku wengi wao wakiishia kuomba msaada barabani.
Licha ya hayo, kuna watu wanaojaribu kubadili dhana hii na kuleta tumaini la maisha kwa watoto hawa waliokata tamaa.
Katika mtaa wa Likoni mjini Mombasa, mchungaji Ernest Mbeva amebadilisha maisha ya watoto na vijana wengi katika eneo hilo kwa kuanzisha makao ya watoto mayatima, yanayoitwa 'Likoni Aids Orphanage Centre'.
Akiongea na mwandishi huyu katika makao hayo siku ya Jumatatu, Mbeva alisema kuwa alianzisha makao hayo kwa kutumia fedha zake kabla ya kutafuta msaada kutoka kwa watu binafsi.
“Nilianza na watoto 12 na wakati huo washirika wa kanisa wakawa wananisaidia kidogo. Baadae nilikodi nyumba ambapo niliamua kuishi nao kama watoto wangu,” alisema Mbeva.
Mchungaji huyo alianzisha makao hayo mwaka wa 2011, na sasa yuko na jumla ya watoto 36 anaowagharamia mahitaji ya kimsingi ikiwa ni pamoja na nguo, malazi pamoja na kuwalipia karo shuleni.
Panjo Josphat, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya Moi Forces, alielezea jinsi mchungaji huyo alisaidia kubadilisha maisha yake.
“Mchungaji Ernest alinichukua nikiwa mdogo baada ya wazazi wangu kufariki na tangu wakati huo, yeye ndiye anayenilipia karo ya shuleni na nina matumaini ya kufaulu maishani,” alisema Panjo.
Kwa sasa Mchungaji huyo hutegemea mashirika pamoja na wahisani wanaojitolea kutoa misaada mbalimbali.
“Haya makao yamesaidia vijana wengi sana. Wengine kwa sasa wanasoma chuo kikuu na wengine ni walimu,” alisema Mbeva.
Kenya imetajwa kama taifa la tatu duniani lenye idadi kubwa ya watoto wanaobaki mayatima baada ya wazazi kufariki kutokana virusi vya ukimwi.
Hatua ya mchungaji Ernest Mbeva ni mfano wa jinsi watu binafsi pamoja na mashirika humu nchini yanavyoweza kushirikiana na kubadilisha taswira hii na kuweka tumaini miongoni mwa watoto hao.