Mashahidi wawili wametoa ushahidi mahakamani Mombasa kuhusu kesi dhidi ya raia 12 wa kigeni waliokamatwa bandarini Mombasa miaka miwili iliyopita kwa madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Shahidi wa kwanza ambaye ni afisa mkuu katika maabara ya wizara ya madini Joram Wambua ameambia mahakama kuwa sampuli zilizotolewa katika meli zilibainika kuwa madini aina ya gypsum na kusema hazikuwa dawa ya kulevya.
Shahidi wa pili Wilfred Kagimbi ambaye ni meneja wa mamlaka ya masuala ya baharini, amesema hawezi kutambua vyema meli inayohusishwa na kusafirisha dawa za kulevya kwani hakupata fursa ya kuikagua.
Kagimbi amesema aliagiza wafanyakazi wengine wa cheo cha chini katika mamlaka hiyo kufanya ukaguzi.
Mashahidi wengine watano wanatarajiwa kutoa ushahidi Alhamisi.
Raia hao 12 kutoka Pakistan, India na Iran walikamatwa mwezi Julai mwaka 2014 bandarini Mombasa kwa madai ya kulangua dawa za kulevya aina ya heroin na pia kumiliki meli iliyosafirisha dawa hizo.
Mahakama ilielezwa kuwa walisafiri kutumia meli kwa jina AL NOOR iliyotia nanga bandari ya Mombasa mwezi huo wa Julai mwaka 2014 ikiwa na zaidi ya kilo elfu 35 za dawa za kulevya aina ya heroin za thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Meli hiyo ililipuliwa mwaka 2014 ikiwa na dawa za kulevya kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta.