Imebainika kuwa meli ya MV Bushehr Amin Darya iliyozamishwa baharini ilikuwa na madini aina ya gypsum wala sio dawa za kulevya kama inavyodaiwa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mtafiti kutoka maabara ya serikali Joram Wambua, aliambia mahakama siku ya Jumatano kuwa waligundua madini ya gypsum walipofanya utafiti wa chemikali zilizopatikana ndani ya meli hiyo.

Wambua aliongeza kuwa hana ufahamu kuwa meli hiyo ilikuwa na heroini.

Itakumbukwa mkuu wa polisi wa kituo cha Kilindini Simon Simotwa aliiambia mahakama kuwa yeye pamoja na wenzake waliikagua meli hiyo kwa mara ya kwanza iliposhikwa baharini na hawakuona dawa za kulevya.

Mwaka jana, Athuman Alfan, ambaye ni afisa wa wanamaji aliiambia mahakama kuwa aligundua meli ya MV Bushehr Amin Darya ilikuwa imebeba dawa hizo baada ya kufanyiwa uchunguzi bandarini kinyume na alivyoambiwa kuwa imebeba saruji pekee.

Hatahivyo, Kipkorir Keteri, alitofautiana na tarehe iliyoandikwa kwenye nakala ya mashtaka, na kusema kuwa meli hiyo ilifika bandarini Mombasa Julai 3, 2014, wala sio Julai 2, 2014.

Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya ambapo wanadaiwa kunaswa na dawa za kulevya bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.

Itakumbukwa meli hiyo ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.