Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu kilimo katika bunge la kumi John Mututho sasa ametaka ushirikiano wa washika dau ili kuweza kukabiliana na mmea wa gugu maji ambao umevamia ziwa Naivasha.

Mututho alisema kuwa mmea huo unasambaa kwa haraka na  kuwa wadudu wa aina ya mende wanafaa kuletwa eneo hilo ili kukabiliana nao.

Wadudu hao hula mmea huo huku mbunge huyo wa zamani wa Naivasha akisema kuwa hilo litakuwa suluhisho.

“Ni wadudu hao tu ndio suluhisho ya tatizo la gugu maji hili, na jambo hili lazima lichukuliwe kwa udharura manake mmea huu unasambaa kwa kasi,” Mututho alisema.

Akiwahutubia wanahabari mjini Naivasha Jumatano, Mututho alisema kuwa ardhi inayopakana na ziwa hilo pia inafaa kuachwa ili mimea inayokua sehemu hizo izuie kemikali kuingia ziwani humo.

Haya yalijiri huku wavuvi wa ziwa hilo wakilalamikia hatua ya afisa mkuu wa maswala ya uvuvi katika kaunti ya Nakuru kwa kuingilia maswala ya wavuvi hao.

Kulingana nao, afisaa huyo ambaye anaelekea kustaafu amekuwa akihujumu juhudi za kupambana na wavuvi haramu tukio ambalo limepelekea kuongezeka kwao.