Meneja wa kampuni ya usambazaji umeme nchini KPLC tawi la Nyamira Dancan Machuka amewahimiza wakazi wa kaunti ya hiyo ambao hawa stima katika nyumba zao kujisajili ili kupokea umeme.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu na mwanahabari huyu, Machuka alisema kuwa yafaa wakazi wajisajili kupokea nguvu za umeme kwa maana viwango vya bei kwa wateja kuunganishiwa zimepungua.
"Serikali ilipunguza pakubwa pesa zinazohitajika kwa mtu yeyote kuunganishiwa umeme katika nyumba yake kutoka elfu 35 hadi elfu 15, na kwa maana hiyo watu wanastahili kujitokeza na kujisajili kupokea umeme ili kujiendeleza," alisema Machuka.
Machuka aidha aliongeza kwa kuwahimiza wateja ambao tayari nyumba zao zimeunganishiwa umeme kuhakikisha kwamba wanatumia umeme kwa umakinifu.
"Ningependa kuwasihi wateja ambao tayari wameunganishiwa umeme kwenye nyumba zao kuhakikisha kwamba wanatumia umeme kwa njia inayofaa ili kulinda matumizi ya umeme," aliongezea Machuka.