Mganga mmoja viungani mwa Maseno amedai kuwahudumia wahubiri kupitia mbinu zake za kiasili.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mzawa wa Alego, Siaya Samuel Tendeka Ndunde almaarufu 'Daktari Eshuya' anayehudumu mtaani Miyekhe kule Maseno amesimulia jinsi wahubiri na watu tajika wanaohudumu katika makanisa mbalimbali hufika kwake kuhudumiwa kwa dawa za kiasili na mbinu nyinginezo za mzuka anazomiliki kikazi.

“Mimi nimewahudumia wahubiri kwa miaka mingi sana, wao huja hapa kwa shida makanisani au dhidi ya mahasimu wao,” Tendeka alisema wakati wa mahojiano pahali pake pa kazi.

Aliongeza, “Ikiwa ni uhasama wa kuhatarisha maisha ya mteja wangu, mimi humuangamiza huyo adui wake.”

Halikadhalika, Tendeka alitaja kuwa baadhi ya watu mashuhuri, mawakili na wakwasi mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti nchini wamekuwa wateja wake kwa muda mrefu. Kulingana naye, hii ni kwa sababu ya huduma yake inayoridhisha.

“Mimi si daktari bandia, mzuka wangu (unaojulikana kama juogi katika Kiluo) huniongoza katika kila hatua ninayoichukua ninapohudumia wateja wangu,” alisema Tendeka huku akikana kulaghai yeyote tangu alipoanza shughuli zake za utabibu mwaka wa 1977.

Katika juhudi za mwandishi huyu kutaka kujua ikiwa ana cheti kutoka kwa idara husika ya serikali, Tendeka alisisitiza kuwa hangeweza kuhudumu miaka kiasi hiki bila ya idhini ya serikali.

Aliweka wazi kuwa hangeweza kuonyesha cheti chochote kama sio tu kwa wawakilishi wa serikali yenyewe. Daktari huyo mwenye makao yake viungani mwa Maseno alieleza kuwa ni lazima ahudumie angalau mtu mmoja katika siku yoyote ile ndipo awe na afya dhabiti.

Alisema, “Hii kazi nimerithi kutoka kwa babu yangu, sijanunua popote. Siku moja ikiisha kama sijafanya huduma yoyote nitaugua.”

Wakati wa mahojiano haya, Tendeka alikuwa na mwanamke mmoja katika chumba chake cha huduma aliyejitambulisha kama mteja wake.

Mwanamke alidai mwanawe mchanga alitibiwa kwa mafanikiomiezi kadhaa iliyopita.

“Kabla nije kwake, niilikuwa nimetembea hospitali tatu kuu hapa Nyanza bila matumaini ya kupata uponyaji kwa mtoto wangu,” alisema mteja huyo.

Tendeka alisema kuwa uchawi hautibiwi hospitalini na ndio maana dawa za kiasili zinathaminiwa sana hata na baadhi ya madaktari wa kisasa na wahubiri aliowahudumia. Hata hivyo, alikana kuwa na uwezo wa kutibu ukimwi.