Maafisa wa utawala katika Kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini leo alasiri wamefanikiwa kumtia nguvuni mpishi sugu kwa pombe haramu katika eneo la Rurii kata ndogo ya Menengai na kunasa zaidi ya lita 30 za chang’aa na zaidi ya lita 1,500 za kangara.
Maafisa hao wakiongozwa na afisa wa tarafa ya Kiamaina, Njuno Macharia pamoja na kamanda wa polisi tawala katika kaunti ndogo hiyo Moses Lekakeny, walimfumania mpishi huyo anaye fahamika kwa jina la utani Gakumbi katika handaki lake la kupikia vileo haramu na kumkamata.
Polisi walipata bidhaa zinazo tumiwa kutengeneza pombe hiyo zikiwemo mapipa 12 ya lita 130 ambayo yalikuwa na pombe ya kangara iliyokuwa ikitayarishwa.
Chang’aa ilikuwa imewekwa kwenye mitungi na ilikuwa moto ishara kuwa ilikuwa imekamilika kupikwa na kupakiwa ili iweze kusafirishwa.
Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bahati akingoja kufikishwa mahakamani hapo kesho.
“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu mno shughuli za jamaa huyo ndiposa tumefanikiwa kumnasa leo. Nawashukuru wananchi wa eneo hili kwa ushirikiano wao kutika kufanikisha vita dhidi ya vileo haramu katika kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini,” alisema bwana Lelakeny.
Kamanda huyo aliwahimiza wananchi kuendelea na ushirikiano huo ili kuhakikisha upishi na unywaji wa pombe haramu umekoma katika eneo hilo.
Aidha inaaminika Gikumbu amekuwa akitayarisha pombe hiyo kisha kuisambaza katika maeneo jirani yakiwemo Nakuru mjini.
Maafisa hao walisisitiza kujitolea kwao katika vita hivyo.