Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mgonjwa aliyemshambulia kwa kisu na kumuua muuguzi aliyekuwa akimhudumia hospitalini, Ijumaa alifikishwa katika mahakama kuu ya Nakuru, huku madai yakichipuka kwamba huenda marehemu hakuwa amesajiliwa kama mhudumu wa kimatibabu.

Mshukiwa George Mungai mwenye umri wa miaka 35, aliishangaza mahakama hiyo alipokiri kumuua muuguzi huyo kwa kutumia kisu cha jikoni. 

Jaji Anthony Ndung’u, alimweleza mshukiwa kuwa hahitajiki kujibu mashtaka hadi afanyiwe uchunguzi wa akili.

Mungai alitekeleza mauaji hayo mnamo Jumanne katika kitongoji cha Machine, viungani mwa mji huu wa Nakuru.

Alimdunga kisu kwenye shingo mhudumu huyo, ambaye alifariki wakati akipelekwa katika hospitali ya Nakuru level five.

Katibu wa chama cha wauguzi tawi la Nakuru, Bi Cyprine Odera, alisema marehemu Monica Wangui ambaye amekuwa akipeana dawa kwa wagonjwa kwa zaidi ya miaka mitano hayuko kwenye sajili zao kama mhudumu wa kimatibabu.

Alisema kulingana na ripoti zao, marehemu alikuwa karani katika kliniki mjini humu baada ya kukamilisha mafunzo ya uuguzi.

Mshukiwa aliwekwa rumande katika gereza la Nakuru hadi Machi 3, ambapo atafika katika mahakama hiyo kujibu mashtaka.