Mhududumu mmoja wa bodaboda amejeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa katika eneo la Freretown na wezi waliojihami kwa silaha butu.
Akizungumza katika kituo cha kuegesha pikipiki eneo la Katisha, Richy Mwambogo anayehudumu katika eneo hilo alisema kwamba kundi hilo linalojumuisha vijana watatu lilimpiga mwenzao huku wakitaka kutoweka na pikipiki yake.
Mhudumu huyo kwa jina Nicholas Kibe alivamiwa alipokuwa akiendelea na shughuli zake karibu na sehemu iliyotengwa ya kutupa taka huko Mgongeni.
Kulingana na Kibe, wahalifu hao walikuwa wamejificha kabla ya kujitokeza kwenye barabara na kumtishia kumuua endapo hangeiwacha pikipiki yake.
Alisema kuwa wezi hao walitoroka baada ya kumulikwa na taa za gari lililokuwa linapita na kumuacha na majeraha, huku wakitoroka na baadhi ya vipuri vya pikipiki.
Alilalamikia hali ya wahudumu wa pikipiki haswa wanaoendesha shughuli zao nyakati za usiku kuvamiwa na makundi ya watu wanaojihami kwa panga na visu.