Mwanamume mmoja ameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kutatiza msafara wa Naibu Rais William Ruto.
Naul Abdalla anadaiwa kutatiza msafara huo katika eneo la Changamwe siku ya Jumatano usiku, naibu rais alipokuwa akielekea katika Ikulu ya Mombasa kutoka Uwanja wa ndege wa Moi.
Mahakama ilielezewa siku ya Alhamisi kuwa Abdalla, ambaye ni mhudumu wa bodaboda, alikataa kusimama na kupisha msafara huo baada ya kusimamishwa na afisa wa trafiki.
Bwana Abdala alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Martin Rabera na kuiambia mahakama alikuwa amechanganyikiwa baada ya kuuona msafara huo.
Hakimu Rabera aliagiza mshukiwa huyo kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu tano.
Kesi hiyo itasikizwa tarehe 30, mwezi Agosti.