Mradi wa serikali wa kujenga kivukio cha magari kwenye makutano ya barabara ya Nakuru-Eldoret na Kericho-Kisumu umepelekea kukwama kwa shughuli za kibiashara katika eneo la Total baada ya mijengo kubomolewa ili kutwaa nafasi kwa mradi huo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya makaazi ya wenyeji pamoja na maduka ya biashara yanaendelea kubomolewa hatua ambayo imepelekea shughuli za kawaida kukwama huku wafanyibiashara wakibaki kuwaza hatima ya biashara zao.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia al maarufu World Bank na kutekelezwa na kampuni moja ya Kichina unatazamiwa kupunguza msongamano wa magari haswa yale yenye uzani mkubwa katika barabara hizo.

Licha ya wengi wa wawekezaji katika kituo hicho cha kibiashara kufidiwa na kukumbatia mradi huo, baadhi ya wamiliki wa ploti na mijengo wamelalama kuwa huenda mali yao ikaharibiwa kabla hawajapata fidia kutoka kwa kampuni husika.

Lucy Wambui ambaye aliongea na wanahabari kwa niaba ya wamiliki wa ploti na nyumba ambao hawajapata fidia, amesema kuwa makaazi yao ni miongoni mwa maeneo ambayo yatabomolewa ili kutoa nafasi ya ujenzi wa kivukio cha magari.

Wenyeji hao wamdai kwamba wamefuatilia fidia hiyo hadi jijini Nairobi na huku mradi huo ukianzishwa wangali wanahangaika bila ya kujua hatima ya mali yao.

Huku hayo yakijiri wakaazi hao wameitaka kampuni inayotekeleza mradi huo kuwapa kazi wenyeji wa eneo hilo haswa vijana ili kukidhi mahitaji yao.

Wamesema ni sharti ujenzi wa barabara hiyo uwape nafasi wenyeji wa eneo hilo wakisema watakumbatia mradi huo iwapo vijana watapata nafasi za kazi.