Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa imetoa ilani kuwa huenda ikalazimika kufunga mikahawa midogo kutokana na tishio la ugonjwa wa kipindupindu.
Hatua hii inajiri baada ya visa vya kipindupindu kuripotiwa katika kaunti hiyo katika siku za hivi majuzi.
Akizungumza alipozuru wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Pwani siku ya jumapili, Mkuu wa Idara ya Afya Mohammed Abdi alisema kuwa huenda uamuzi huo ukaafikiwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari.
“Tayari zaidi ya watu 60 wanaougua kipundupindu wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali Kuu ya Pwani,” alisema Abdi.
Abdi pia alisema kuwa tayari mikakati zinawekwa ili kuhakikisha kuwa maji ambayo wakaazi wa kaunti hiyo wanatumia imetibiwa vilivyo kama njia moja ya kukabiliana ugonjwa huo.