Serikali ya Kaunti ya Kisii, kupitia sekta ya Afya na ya Elimu wameweka mikakati kabambe ya kupambana na magonjwa ya macho, na kuwaomba wakazi wote wa kaunti hiyo na viunga vyake kushirikiana nao ili kupigana na magonjwa hayo.
Akiongea hii leo katika shule ya msingi ya Kisii katika hafla ya kupeana vyeti kwa waliofuzu katika mafunzo ya kukabiliana na magonjwa ya macho, Daktari mkuu wa macho katika hospitali ya Kisii Clarice Onyango aliwaomba watu wote kushirikiana ili kutambua shida za macho hasa kwa watoto kuanzia mwaka mmoja hadi 15.
Onyango alisema kuwa kutokana na ushirikiano wao na wafadhili walioleta funzo hilo lililoanza mwaka wa 2013 na litakalokamilika mwaka wa 2016, shirika la Briehholder vision Institute, likishirikiana na Conjuction Operational Eyesight Institute walitoa mafunzo hayo kwa walimu 91, wahudumu wa afya 50 na wahadumu wa afya ya Jamii 33, ambao walipokezwa vyeti vya kufuzu hii leo.
“Leo tumepeana vyeti kwa walimu pamoja na wahudumu wa afya ambao wamehitimu kutokana na funzo tulilokuwa nalo jinsi ya kutambua magonwa hayo na kwa sasa wataenda kutusaidia pakubwa,” alihoji Onyango.
Daktari alisema kuna magonjwa mengi ya macho yanawasumbua watoto wachanga ambayo yanastaili kupata tiba la mapema.
Kutokana na uchunguzi uliofanywa tangu funzo hilo lianzishwe, watoto 340 walipatikana wamehadhirika na magonjwa ya macho, kati ya watoto 2,000 walioachunguzwa.
Aidha, alisema magonjwa kama hayo huchangia kufeli kwa mwanafunzi hasa wakati wanapokuwa na shida ya kuangalia ubao.
“Magonjwa kama hayo yanaweza kuchangia kufeli kwa mwanafunzi kwa kuwa huwa na shida ya kuona hasa katika ubao,” aliongezea Daktari.