Kaunti ya Uasin-Gishu inapanga kutumia shilingi milioni 25 kukarabati vibanda vya wafanyibiashara sekta ya juakali mjini Eldoret.
Mbali na kukarabati vibanda hivyo utawala huo unapanga kutumia sehemu ya fedha hizo kupanua masoko pamoja na kuongeza masoko zaidi mbali na kujenga masoko yenye hadhi ya kisasa.
Iwapo bajeti hiyo itapitishwa bungeni serikali hiyo itajenga masoko manne zaidi katika kila kaunti ndogo Uasin-Gishu.
Waziri wa biashara ,utalii na ustawi wa vyama vya ushirika katika kaunti hiyo Paul Melly alisema Jumanne hii kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa mbinu ambazo kaunti hiyo inabuni ili kupunguza msongamano wa wachuuzi katikati mwa mji wa Eldoret.
"Tunapanga kutumia hizi pesa kujenga masoko matatu mapya ya kisasa viungani mwa mji wa Eldoret ,vile vile tunapania kukarabati masoko manne na kuyapatia sura mpya ili kuboresha na kupanua sekta ya juakali katika kaunti hii," alisema Melly
Wakati huo huo Melly alitaka wafanyibiashara katika sekta ya juakali mjini Eldoret kujiunga na vyama vya ushirika ili kuboresha maisha yao.
utawala wa kaunti hiyo unashirikiana na wahudumu wa pikipiki za uchukuzi wa abiria al maarufu boda boda ili kuona kwamba wahudumu husika wamejiunga na vyama vya ushirika.
Kwa mujibu wa Melly ni kwamba zaidi y wahudumu 3,000 wa bodaboda wanahudumu mjini humo ambapo wanapaswa kujiunga na chama cha ushirika.
Alisema iwapo wahudumu hao watajiunga na vyama vya ushirika kutakuwa na ustaarabu katika sekta ya bodaboda.