Utafiti uliofanywa na idara ya afya Kaunti ya Mombasa umebaini kuwa mitaa ya mabanda ndiyo inayoongoza katika maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Afisa wa afya anayehudumu katika mtaa wa mabanda wa Moroto, eneo la Tudor, Asia Nduta, amesema kuwa idadi ya wagonjwa wanaougua kifua kikuu imeongezeka katika mitaa hiyo kufuatia mazingara duni.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne, Nduta alisema kuwa hali hiyo imetokana na ujenzi duni wa nyumba, sawia na kutofahamu umuhimu wa usafi wa mazingira.
Afisa huyo aliwahimiza wakaazi kukodi nyumba zilizo na nafasi ya kupitisha hewa safi.
"Tunawaomba wakaazi kuzingatia mazingira safi pamoja na kuishi kwa nyumba zilizo na hewa safi ili kuthibiti kuenea kwa ugonjwa wa kifua kikuu,” alisema Nduta.
Nduta alisema kuwa umaskini katika jamii pia umechangia ongezeko la ugonjwa huo, na kuwashauri wakaazi kuzingatia lishe bora pamoja na kuhifadhi mazingira ili kuepukana na kuenea kwa ugonjwa huo wa kifua kikuu.
Juma lililopita, Shirika la Msalaba Mwekundu Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na idara ya afya ilitoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa kijamii kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu na jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo.