Wanabodaboda wote katika mji wa Kisii na viunga vyake wameombwa kuwa na uwazi na wateja wao hasa wakati wakulipwa na wateja wao ili kuepuka mizozo ya pesa na wateja wao.
Wakiongea katika eneo la Mashauri kaunti ya Kisii, baadhi ya wateja walilalama kuwa wanabodaboda wengi huwa vigeugeu kwa wateja wao wakati wamewafikisha wanakoenda na kuwadai pesa zaidi ya walizoelewana.
“Nimeghadhabishwa na mwanabodaboda ambaye alinibeba asubuhi ya leo kutoka kituo cha Menyikwa na kunifikisha hapa kwa sababu alinidai pesa zaidi ya tulizoelewana naye kutoka Menyikwa,” alisema James Gichana mwanafunzi wa chuo kimoja mjini Kisii.
Aidha amewaomba wanabodaboda hao kuwa na uwazi wanapopewa pesa hasa noti na kurudisha salio kulingana na jinsi walivyoelewana na mteja wake.
“Tunajua pikipiki katika usafiri ni haraka kuliko gari kwa kuwa mimi kama mwanabiashara huwa nataka kufika sokoni mapema kwa hivyo ninaomba wanabodaboda na sisi kama wateja kuelewana ili uchukuzi katika mji wetu uendelee vizuri,” alihoji Jospheni Gesare mwanabiashara .
Kwa upande wa wanabodaboda wamewalaumu wateja wao kwa kile walisema kuwa wateja wao huelewana bei na wakati wanawafikisha mahali walielewana, wateja wao ugeuka na hutoa pesa kidogo .
“Tunaelewana bei na wateja wetu lakini tukiwafikisha mahali wanastahili kufikishwa hugeuka na kutoa pesa kidogo sisi wanaboda boda ndio twawekewa lawama si mteja,’’alielezea Fred Bosire mwanabodaboda.
Wanabodaboda hao wamewaomba wateja wao kuwajibika na kazi yao ili kuepuka na mizozo kama hiyo.