Huku shughuli za mazishi za aliyekuwa mwanabiashara maarufu Jacob Juma zikiendelea, mjane wake Miriam Wairimu sasa anataka maajenti wa kimataifa wanaohusika na uchunguzi kusaidia kukitegua kitendawili kinachokumba mauaji ya baba huyo wa watoto wawili.
Kati ya wataalamu ambao mjane Miriam anataka wasaidie katika uchunguzi huo ni wale wa shirika la ujasusi la FBI, Scotland Yrad pamoja na wachunguzi wengine wa kibinafsi.
Katika taarifa kwa wanahabari Ijumaa asubuhi kabla ya mwili wa Juma kusafirishwa hadi uwanja wa ndege wa Wilson na kisha Kakamega, Bi Miriam, aliyekuwa ameandamana na kinara wa Cord Raila Odinga, alihoji; “ni kwa nini polisi wa kituo cha Karen hawakukimbia kulinda eneo hilo baada ya mkasa ili kuzuilia ushahidi”.
Aidha ametaka maafisa wa polisi kuipatia familia hiyo “video ya kamera za siri (CCTV) zinazoonyesha vile kitendo hicho kilifanyika, na nambari za usajili wa gari lililompeleka marehemu Juma katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.
“Juma alikuwa na stakabadhi zote za utambulisho wake, na pamoja na wakaazi wengine, walijulikana vizuri na polisi wa kituo cha Karen. Pia tunataka kujua saa ambazo kisa hicho kilifanyika na mwili wake ulipofikishwa kwenye chumba cha maiti” akasema Bii Wairimu Juma.
Aidha anasisitiza kwamba polisi hawakumwambia kuhusu kifo cha mumewe, hadi alipopeleka watoto wake shuleni ndipo akasikia habari hizo kutoka kwa wazazi wenzake.
Pia amemtaka waziri wa maswala ya ndani Joseph Nkaissery na inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet kuwapa rekodi za simu yake ya rununu usiku huo wote.