Mji wa Mombasa uko katika hatari ya kuzama kwenye mitaa ya vitongozi duni iwapo mipangilio ya haraka haitaidhinishwa kuliboresha jiji hilo lenye maadhari ya kuvutia ya kitalii.
Akizungumza katika mkutano na wadau mbalimbali wa sekta za umma na kibinafsi za kimazingira mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mipangilio wa mji kaunti ya Mombasa Francis Thoya alisema kwamba lazima kwa wadau hao kuibuka na mbinu mbdala za kudhibiti mji huo.
Kulingana na Thoya, hali iliyopo kwa sasa ya vitongoji duni hadi katikati mwa Jiji hilo inastahili kufanyiwa ukaguzi wa kina na kurekebishwa mara moja kabla ya Jiji hilo la Mombasa kusheheni vitongoji duni.
Alisema kwamba hali hiyo imechangiwa na ujenzi wa kiholela ambao haujazingatia sheria za miundomsingi ya mji huo, huku akisema kwamba ni lazima wakazi wa kaunti hiyo wakubali na waruhusu serikali ya kaunti hiyo kutekeleza mipangilio yake ili kuzuia ujenzi wa kiholela.
"Mji wa Mombasa umesheheni vitongoji duni hadi katikati mwa jiji, na hali hii iwapo haitashughulikiwa kwa dharura, basi maandhari ya kuvutia ya kitalii ya jiji hili itaangamizwa kutokana na hali duni ya kimazingira tunayoishuhudia kwa sasa. Ni lazima wakazi wakubali kuipa serikali yetu ya kaunti nafasi ili kuukarabati mji huu,” alisema Thoya.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hezel Katana alisema kwamba kuna haja ya wakazi kuhamasishwa kuhusiana na umuhimu wa mpangilio wa mji huo ili wasiathirike na mafuriko, uharibifu wa mazingira na hasara ya kubomolewa majumba yao yanayojengwa kiholela.
Mji wa Mombasa tayari una mitaa ya mabanda inayokuwa kwa kasi ukiwemo ule wa Moroto katika eneo la Tudor, Bangladesh katika eneo bunge la Jomvu na maeneo ya Chaani.