Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mji wa Mombasa umeteuliwa katika tuzo za kimataifa za utalii maarufu kama World Travel Awards mwaka huu wa 2016.

Mji huo wa kitalii umeteuliwa kushindania nafasi ya eneo bora la kuzuru barani Afrika ambapo utapata ushindani mkubwa kutoka kwa miji ya Johannesburg na Durban zote za Afrika Kusini miongoni mwa miji mingine.

Mbali na mji huo, pia Bandari ya Mombasa imebahatika kuteuliwa katika tuzo hizo kuwania nafasi ya Bandari bora Afrika inayosafirisha watalii.

Bandari hiyo ya Mombasa imeteuliwa katika nafasi moja na ile ya Dar-es-salaam nchini Tanzania, Port Elizabeth ya Afrika kusini miongoni mwa zingine.

Uteuzi wa mji pamoja na Bandari ya Mombasa katika tuzo hizo za kimataifa umeleta taswira mpya katika sekta ya utalii nchini huku kukiwa na matumaini kwamba juhudi za kuimarisha sekta hiyo zinazidi kutambulika.

Mombasa ni mji wenye historia na tamaduni za aina yake ambazo huwavutia wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Bandari ya Mombasa ambayo imeteuliwa kuwania tuzo za Bandari bora Afrika pia imekuwa ikitekeleza jukumu kubwa katika kuingiza na kusafirisha bidhaa mbalimbali huku ikiwa ndio bandari inayotegemewa zaidi ukanda wa Afrika mashariki.

Katika kitengo cha sehemu bora ya kutalii baharini, ufuo wa bahari wa Diani uliopo pia katika ukanda wa Pwani ya Kenya umeteuliwa ambapo umeshindanishwa na ufuo wa Zanzibar nchini Tanzania, Cape Town Afrika Kusini miongoni mwa zingine.

Tuzo za World Travel Award zilizinduliwa rasmi mwaka wa 1993 kwa lengo la kutambua na kutuza kampuni pamoja na miji mbalimbali inayotoa mchango katika sekta ya utalii duniani.

Zaidi ya miji pamoja mashirika 1,500 yameteuliwa katika tuzo za mwaka huu huku hafla ya kutawaza washindi ikitarajiwa kufanyika tarehe Aprili 9 katika ukumbi wa Diamonds la Gemma huko Zanzibar nchini Tanzania.