Mkalimani mmoja wa lugha ya Kifarsi amekanusha madai ya kutishiwa maisha kwenye kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Hussein Hassan, anayefanya kazi katika afisi za Ubalozi ya Marekani jijini Nairobi, ameiambia mahakama kuwa hajatishiwa maisha na mtu yoyote yule.
Hassan alisema kuwa alikosa vikao vya kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya inayomkabili mwana wa Akasha na wenziwe kutokana na shughuli nyingi za kikazi jijini Nairobi.
Aidha, Hassan alielezea mahakama siku ya Jumatatu kuwa alikuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hivyo basi hakuweza kusafiri hadi Mombasa kuhudhuria vikao vya kesi hiyo.
Hii ni baada ya Mahakama ya Mombasa kumtaka kuelezea sababu iliyomfanya kukosa vikao zaidi ya viwili vya mahakama.
Kulikuwa kumezuka tetesi kuwa mkalimani huyo ametishiwa maisha na watu wasiojulikana na kumuonya kutohudhuria kesi hiyo.
Ibrahim Akasha na wenziwe watatu wanakabiliwa na kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroini.