Huku ulimwengu unapoadhimisha siku ya kifua kikuu duniani, mke wa gavana wa kaunti ya Nyamira Naomi Nyagarama amejitokeza kuwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kutembelea vituo vya kimatibabu ili kujua iwapo wameathirika.
Akiwahutubia wakazi wa Ekerenyo siku ya Alhamisi, Nyagarama alisema kuwa yafaa watu watembelee vituo vya afya ili kupimwa kujua iwapo wameathirika.
"Kitu ambacho watu wanastahili kujua ni kwamba ugonjwa wa kifua kikuu una tiba iwapo itagundulika mapema kuwa mtu ameathirika ili utibitiwe, na ndio maana nawahimiza wakazi wa kaunti hii kutembelea vituo vya afya ili wapimwe kujua iwapo wameathirika na TB," alisema Nyagarama.
Aidha aliwahimiza wakazi wanaoishi na ugonjwa wa ukimwi kuendelea kunywa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi mwilini.
"Kwa wale watu ambao wameathirika na ugonjwa wa ukimwi ningependa kuwarahi waendelee kunywa dawa za kupunguza makali ya virusi vinavyosababisha ukimwi ili waendelee na maisha yao kama kawaida," aliongezea Nyagarama.